SERIKALI IHARAKISHE MCHAKATO UTUNGAJI SHERIA MAALUM KULINDA HAKI ZA WAZEE – THBUB

Na Gideon Gregory – Dodoma.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imeiomba Serikali iharakishe mchakato wa kutunga sheria maalum ya Wazee, ili kulinda haki zao kisheria kutoana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

Pendekezo hilo limetolewa leo Jun 15,2025 na Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu wakati akitoa tamko kwa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kupinga ukatili dhidi ya Wazee iliyokwenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Wazee ni Hazina kwa Taifa, Tuwalinde, Tuwatunze.

“Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote katika kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani, ambayo inaikumbusha jamii umuhimu wa kuwaenzi, kuwasikiliza wazee sambamba na kuacha vitendo vya ukatili, manyanyaso na udhalilishaji dhidi ya wazee,” amesema.

Amesema THBUB inatambua jitihada na mchango wa Serikali ya katika kuboresha maisha ya wazee, ikiwemo kuwapatia huduma jumuishi na stahiki kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao, kuongezeka kwa kiwango cha chini cha pensheni, utoaji wa huduma za afya kwa wazee na ujenzi wa makazi ya wazee katika maeneo 13 nchini.

“Jitihada nyingine ni npamoja na kuunganishwa kwa wazee katika mfuko wa TASAF, kuorodheshwa katika makundi maalum ya namna ya kupata zabuni za Serikali na hivi karibuni Serikali imeanzisha vikundi 395 vya uzalishaji Mali vya wazee kwa wazee 10,926,”amesema.

Aidha, Mhe Mwaimu ameongeza kuwa THBUB inatambua jitihada na mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweka utaratibu wa kuwapatia pensheni na vitambulisho vya kupatiwa huduma mbalimbali wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70 na kutunga Sheria ya Masuala ya Wazee Na. 2 ya mwaka 2000.

Pia Serikali imependekea Serikali ishirikiane na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa jamii kuachana na ukatili dhidi ya wazee pamoja na wananchi wote kwa ujumla kulinda na kutetea haki za wazee ikiwemo kuthamini mchango, uzoefu na ushiriki wao kwa maendeleo ya taifa.

“Tume inatoa wito kwa wananchi wote kwa pamoja tutekeleze wajibu wetu kwa wazee kwa kuhakikisha tunawalea, tunawaheshimu, tunawapatia ulinzi, usalama, chakula, mavazi na malazi,”ameongeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *