Na Gideon Gregory – Dodoma.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, amesema Wizara huyo imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususani walioko maeneo ya pembezoni, ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kuwasilisha changamoto za kisheria zinazowakabili kwa lengo la kuboresha huduma na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.
Akitoa mrejesho wa programu zilizopita kupiti mpango wa SEMA NA WAZIRI leo Aprili 22,2026 jijini Dodoma Dkt. Homera ameeleza kuwa programu hiyo imekuwa daraja muhimu kati ya wananchi na serikali katika kutatua migogoro mbalimbali ya kijamii na kisheria.
Amesema tangu kuanzishwa kwa programu hiyo Machi 17 mwaka huu, jumla ya malalamiko 2,277 yamepokelewa na kufanyiwa kazi, huku wastani wa malalamiko 67 yakipokelewa kwa kila kipindi. “Programu hii inaendelea kuwa chombo madhubuti cha kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi popote walipo nchini,” amesema.

Miongoni mwa kesi zilizopokelewa ni ya mwanafunzi Salma Omari kutoka chuo cha DIT Kampasi ya Mwanza, aliyekumbwa na mkanganyiko wa kozi uliomfanya kushindwa kuona matokeo yake. Wizara imeeleza kuwa tayari imewasiliana na uongozi wa chuo husika ili kuhakikisha mwanafunzi huyo anapatiwa haki yake ya kusoma kozi anayoihitaji bila kupoteza muda zaidi.
Miongoni mwa kesi zilizopokelewa ni kuhusu ukatili wa kijinsia, ambapo wizara imelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua za haraka katika tukio la Simiyu lililohusisha mama aliyekuwa akipigwa na mumewe. Mtuhumiwa tayari amekamatwa na anaendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
Akizungumzia mwenendo wa malalamiko, Dkt. Homera amesema migogoro ya ardhi inaongoza kwa asilimia 31.3, ikifuatiwa na ajira (19.4%) na madai (13.4%), huku masuala mengine yakijumuisha mirathi, msaada wa kisheria na ukatili wa kijinsia. Kati ya malalamiko yote, asilimia 56.7 tayari yamepatiwa ufumbuzi.

“Tunawahakikishia wananchi kuwa wizara imejipanga kikamilifu kushughulikia malalamiko yote kwa wakati na kwa ufanisi,” amesisitiza Dkt. Homera, akiongeza kuwa wataalamu wenye ujuzi wa kutosha wameandaliwa kushughulikia changamoto hizo.
Programu ya ‘Sema na Waziri’ inaendelea kurushwa mara mbili kwa mwezi, ikilenga kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan walioko maeneo ya pembezoni, ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki na kusikilizwa.


