Selimundu Haitokani na Kurogwa,Msitumie Mitishamba Kuitibu

Na William Bundala,Kahama

Wazazi na walezi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuacha kutumia dawa za mitishamba kutibu ugonjwa wa Selimundu na kuondokana na imani kuwa ugonjwa huo unatokana na kurogwa.

Wito huo umetolewa Leo na Mkurugenzi wa Daktari Nyumbani App Dr Muselya Kiula wakati akizungumza na Jambo Fm kwenye Kambi ya matibabu ya Kahama Gold City Marathon iliyopo kituo Cha Afya Nyasubi.

Dkt. Kiula amesema kuwa ugonjwa wa Selimundu mtu anarithi kutoka Kwa baba na mama na siyo ugonjwa wa kurogwa na kwamba Kwa Afrika Tanzania ni nchi ya Nne na Kwa Dunia ni nchi ya Tano kuwa na wagonjwa wengi wa Selimundu.

Sambamba na hayo Dkt. Kiula amesema kuwa dalili za Selimundu huonekana mtoto akifikisha miaka tisa kupanda juu ambazo huwa ni pamoja na kupungukiwa damu,kupata homa ya  manjano,changamoto za ukuaji pamoja na kupooza.

Kwa upande wake mratibu wa Gold City Marathon Conrad Nkuba amesema kuwa lengo kubwa la Mbio hizo ni kutoa huduma ya elimu na matibabu ya ugonjwa wa Selimundu bure kwa watoto wanaokabiliwa na tatizo la ugonjwa huo.

Kahama Gold City Marathon itafanyika siku ya Jumapili June 9 katika uwanja wa Magufuli zikitarajiwa kuhitimishwa katika uwanja wa Taifa Kahama lengo kuu likiwa ni kuchangia watoto wenye Selimundu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *