SEKTA YA HABARI NI NYENZO MUHIMU KATIKA KULINDA, KUDUMISHA AMANI KIPINDI CHA UCHAGUZI – DKT. BITEKO

Tasnia ya habari nchini inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kabla na baada ya uhuru ambapo uwepo wa baadhi ya vyombo vya habari vya awali kama vile gazeti la Sauti ya TANU na redio Sauti ya Dar es Salaam vilisaidia kutoa mchango mkubwa katika kujenga umoja, utaifa na kuhamasisha ushiriki wa harakati za kudai uhuru.

Akizungumza leo Julai 9, 2025 jijini Dar es salaam wakati akifungua Mkutano wa Wadau Kujadili Mchango wa Sekta ya Habari katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa waandishi wa habari nchini kuwa walinzi wa ukweli, wajenzi wa amani na wachochezi wa uwajibikaji wa kisiasa.

Sambamba na kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinabaki kuwa kioo safi cha jamii kisicho na doa la uzushi, chuki au upendeleo na kuendelea kuhimiza maelewano, uvumilivu wa kisiasa, na utamaduni wa kuheshimu tofauti za maoni.

“ Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa, waandishi wa habari katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi wanabaki salama wao pamoja na mali zao. Aidha, Serikali, tutaendelea kulisimamia hili kwa nguvu zetu zote. Tutahakikisha kuwa, mnakuwa na mazingira salama, huru na rafiki wakati wote wa majukumu yenu, amesema Dkt. Biteko.

Ameendelea kusema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu 20205 katika jamii kutakuwa na watu wenye mitazamo mbalimbali kulingana na vipaumbele vyao hata hivyo vyombo vya habari vina fursa ya kutoa uelekeo kwa taifa.

“Uchaguzi ni kipindi cha muda mfupi, tumuombe Mungu hata baada ya Uchaguzi tubaki kuwa Taifa moja lenye ustahimilivu na kila mmoja akitoka kwake aende kutafuta mkate arudi nyumbani kwa familia yake kukiwa na amani, sisi kupitia mkutano huu tuungane kuhakikisha Taifa letu linabaki salama. Sekta ya habari ni nyenzo muhimu katika kulinda na kudumisha amani katika kipindi chote cha uchaguzi,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *