Sekta ya Fedha Yaimarika,leseni michezo ya kubahatisha zatolewa kwa asilimia 82

Na Gideon Gregory,Dodoma

Waziri wa Fedha Dkt.  Mwigulu Nchemba amesema hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu Bodi ya Michezo ya kubahatisha imetoa jumla ya leseni 9,805, sawa na ufanisi wa 82% ya lengo la mwaka ambapo kati ya kiasi hicho, leseni 6,261 zimehuishwa na 3,544 ni leseni mpya.

Dkt. Nchemba ameyasema hayo leo Juni 4,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kuongeza kwa mwaka 2023/24, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha ilipanga kutoa leseni 11,880 kwa waendesha michezo ya kubahatisha, ambapo 2,273 ni leseni mpya na leseni 9,607 ni za kuhuisha.

Aidha, Bodi imekagua jumla ya waendeshaji 87 wa michezo ya kubahatisha, sawa na asilimia 86 ya lengo la mwaka. Vilevile, Bodi imeteua kampuni ya kuendesha Bahati Nasibu ya Taifa na tayari imesaini mkataba wa uendeshaji kwa mujibu wa sheria ya michezo ya kubahatisha.

Wakati huo huo Dkt.  Mwigulu Nchemba amesema Sekta ya fedha nchini imeendelea kuwa imara, na vihatarishi kupungua kutokana na matarajio ya uchumi wa dunia kuendelea kuimarika na kuongeza kuwa Sekta ya kibenki ambayo ni sehemu kubwa ya sekta ya fedha imeendelea kuwa imara, yenye kutengeneza faida, ukwasi na mtaji wa kutosha.

“Ubora wa rasilimali uliendelea kuongezeka, ambapo uwiano wa mikopo chechefu ulipungua hadi asilimia 4.3 Desemba 2023 kutoka asilimia 5.5 Juni 2023”, ameongeza.

Pia meongeza kuwa hali hiyo inaashiria kuendelea kupungua kwa vihatarishi katika utoaji wa mikopo kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi pamoja na hatua za kisera na kiusimamizi zinazoendelea kuchukuliwa na benki kuu ili kupunguza mikopo chechefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *