SAM NUJOMA RAIS WA KWANZA WA NAMIBIA AAGA DUNIA

Sam Nujoma, mpigania uhuru ambaye aliiongoza Namibia kupata uhuru kutoka kwa wabaguzi wa rangi ukanda wa Kusini mwa Afrika na kuhudumu kama Rais wa kwanza wa nchi yake, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.

Taarifa ya Rais wa Namibia, Nangolo Mbumba imeeleza kuwa Nujoma amefariki baada ya kuwa amelazwa Hospitalini kwa muda wa wiki tatu zilizopita, akipambana na ugonjwa ambao haukuweza kutajwa mara moja.

“Kwa huzuni na masikitiko makubwa natangaza kufariki kwa mpigania uhuru wetu anayeheshimika na kiongozi wetu wa mapinduzi. Baba yetu Mwanzilishi aliishi maisha marefu na yenye matokeo ambayo alitumikia kwa njia ya kipekee watu wa nchi yake anayoipenda,” alisema Rais Mbumba.

Nujoma alizaliwa katika familia ya Wakulima masikini kutoka kabila la Ovambo, akiwa mtoto wa kwanza kati ya watoto 10, na baadaye alipata kibarua cha ufagiaji wa reli karibu na jiji la Windhoek mwaka wa 1949 alipokuwa akihudhuria masomo ya usiku.

Huko, alikutana na chifu wa kabila la Herero, Hosea Kutako ambaye alikuwa akimshawishi kukomesha utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Namibia, wakati huo ikijulikana kama Afrika Kusini Magharibi.

Kutako akawa mshauri wa Nujoma, akimuongoza wakati alipokuwa akijishughulisha na siasa akiwa ni miongoni mwa wafanyakazi weusi wanaopinga agizo la Serikali la kuhamia mji mpya mwishoni mwa miaka ya 1950.

Kutokana na ushawishi wa Kutako, Nujoma alianza maisha ya uhamishoni mwaka 1960, akimuacha mkewe na watoto wanne na mwaka huohuo alichaguliwa kuwa rais wa Jumuiya ya Watu wa Kusini Magharibi (SWAPO) na kusafiri miji mbalimbali kutafuta uungwaji mkono wa kudai uhuru.

SWAPO ilianzisha mapambano ya kutumia silaha mwaka 1966 baada ya nchi jirani ya Afrika Kusini kukataa amri ya Umoja wa Mataifa ya kuachana na mamlaka yake juu ya koloni la zamani la Ujerumani ikisema kuwa ilikuwa kinga dhidi ya maendeleo ya ukomunisti barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *