Licha ya kwamba Katika michezo sita (6) iliyopita ya ligi dhidi ya Yanga SC hakuna mchezo ambao Dodoma Jiji FC imeshinda, bado timu hiyo imeibwekea Yanga SC na kutamba kuitingisha katika mchezo wao wa jioni ya leo saa 19:00 Azam Complex, Dar es salaam.
Kwani wanasema, wanaingia kwenye mechi hiyo wakiwa kama madaktari wa kichina, penye maumivu ndipo wanapoweka dawa, hiyo ni kutokana na matokeo ya mechi iliyopita ya Yanga SC dhidi ya Kagera Sugar.
“Ni kweli rekodi hazioneshi kufanya vizuri dhidi yao, lakini mpira umebadilika si unaona kinachotokea Afcon, safari hii tumekuja kama madaktari wa kichina sehemu yenye maumivu ndio tunaingiza dawa, watakaposema yalaa ndio hapo hapo labda wakae kimya ndio salama yao” Patrick Semindu Afisa Habari Dodoma Jiji FC.
Timu hiyo inayonolewa na kocha wa zamani wa Kagera Sugar na Biashara United, Francis Baraza, imefanya maingizo kadhaa mapya ikiwemo Anuary Jabir, Robinson Kamura na Apollo Otieno na Abubakar Juma.