Viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) wameidhinisha kutumwa kile wanachosema ni kikosi cha Jeshi cha dharura kurejesha utaratibu wa kikatiba nchini Niger, uvamizi ambao utafanyika haraka iwezekanavyo kumrejesha madarakani Rais Bazoum ambaye alipinduliwa kijeshi.

Akiongea baada ya kurejea kutoka mkutano wa kilele wa Mataifa Wanachama wa ECOWAS uliofayika Abuja nchini Nigeria August 10,2023, Ouattara amesema Wakuu wa Majeshi ya nchi hizo watafanya mikutano mingine kujadiliana hatua zinazoendelea kwenye kampeni hiyo ya kijeshi dhidi ya Watawala wa kijeshi wa Niger.
Bila ya kuzitaja hatua hizo kwa undani, Rais huyo wa Ivory Coast amesema wao kama Viongozi Wakuu wa Nchi walishatoa idhini ya kuanzisha oparesheni na kwamba Nchi yake itachangia Wanajeshi zaidi ya 1,000, ambao watashirikiana na wenzao wa Nigeria, Benin na Mataifa mengine Wanachama wa ECOWAS.
Ouattara amesema Viongozi wa Jumuiya hiyo wamedhamiria kumrejesha madarakani Rais Mohamed Bazoum aliyepinduliwa na Wanajeshi wiki mbili zilizopita na tayari Rais wa Kamisheni ya ECOWAS, Omary Touray, ametangaza kutumwa kwa Wanajeshi wa jumuiya hiyo nchini Niger.