Waziri Wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi H. Chana amesema uwepo wa vitendo vya rushwa kunaifanya Serikali kushindwa kutekeleza ipasavyo jukumu lake la kuwahudumia wananchi ipasavyo na kusababisha miradi ya maendeleo kushindwa kufanyika au kufanyika kwa kiwango cha chini kutokana na fedha zinazotengwa kutekeleza miradi hiyo, kuingia katika mikono ya watu wachache.
Balozi Chana ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, wakati akizindua Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ambapo amesema serikali kupitia TAKUKURU imekuwa ikifanya ufuatiliaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo ili kukabiliana na ubadhilifu ikiwemo rushwa.
Waziri huyo ameongeza kuwa Maadhimisho ya mwaka huu yanaadhimishwa sambamba na maadhimisho ya miaka 75 ya Tamko la Haki za Binadamu ambalo lilitamkwa tarehe 10 Desemba,1948 na kuweka msingi wa mikataba mingine ya Haki za binadamu ambayo imefuata. Kilele cha Maadhimisho ya mwaka huu itakuwa Disemba 10, 2023 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma na yanaongozwa na kauli mbiu ya ‘’Mapambano Dhidi ya Rushwa ‘’Zingatia Maadili, Utu, Uhuru na Haki kwa Watu Wote kwa Maendeleo Endelevu’.
Kauli mbiu hii imekuja wakati muafaka kwani inatufanya tutafakari kwamba ili tupate maendeleo lazima tuzingatie maadili, utu, uhuru na haki za binadamu kwa watu wote ambayo ni masuala ya msingi sana kwa ustawi wa taifa letu na watu wake.