Katika mastaa wapya tisa wa mwisho kusajiliwa na Simba wachezaji wenye viwango vya ukubwa wa klabu hiyo ni wawili tu, Che Malone na Fabrice Ngoma.
Hiyo ndiyo kauli ya mwisho ya Kocha aliyetimuliwa na klabu hiyo, Robertinho kwa mashabiki kupitia kwa Mwanaspoti, dakika chache kabla ya kukwea pipa kuondoka kwenye ardhi ya Tanzania.
Maana yake ni kwamba, Luis Miquissone, Aubin Kramo na kipa Ayoub Lakred, David Kameta ‘Duchu’, Abdallah Khamis, Hussein Kazi, Hussein Abel na Shaaban Idd Chilunda ni wazuri lakini wa kawaida sana lakini hakuwa na namna ingawa amepambana na kupoteza mechi moja tu Msimbazi.
Kocha huyo ameng’olewa Simba kikubwa zaidi ikiwa ni baada ya timu hiyo kula kichapo cha mabao 5-1 dhidi ya Yanga, Jumapili iliyopita Kwenye Uwanja wa Mkapa. Robertinho aliondoka saa 5 usiku wa kuamkia jana, huku akisisitiza kwamba hana kinyongo na Simba lakini Che Malone na Ngoma ndiyo wachezaji wenye viwango bora katika usajili wa mwisho uliofanyika Simba. Kipigo dhidi ya Yanga ni cha kwanza kwake tangu ajiunge na timu hiyo Januari 3 mwaka huu na cha kwanza katika ligi kwa msimu huu pia cha kwanza tangu ilipofungwa na Azam Oktoba 27 mwaka jana.
Simba imecheza mechi 19 za ligi, alisema katika usajili mpya ambao timu hiyo iliufanya msimu huu ni Ngoma na Che Malone ndio wachezaji wenye viwango na waliosalia ni papatu papatu tu!
Nyota hao wameungana na wakali wengine waliokuwepo msimu uliopita ambao Robertinho aliwakuta na kumaliza nao katika nafasi ya pili ya Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga, huku ikitoka kapa kwa kukosa tena mataji matatu iliyokuwa imeyapoteza kwa watani wao, likiwa Kombe la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii.
#Chanzo:Mwanaspot