Mgombea Udiwani wa Kata ya Pasiansi katika jimbo la Ilemela mkoani Mwanza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Regina Lubala, ameahidi kushughulikia changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara katika kata hiyo endapo atapata ridhaa ya wananchi kumchagua kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Regina ameyasema hayo wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika mtaa wa Pasiansi Juu, ambapo amesema barabara nyingi, hususan ile inayoelekea kwenye eneo la makaburi, zimekuwa kero kubwa kwa wananchi kutokana na kukatika na kufanya magari kushindwa kufika maeneo hayo.

“Katika mtaa huo kuna barabara ambayo inapita mpaka kwenye maeneo ya makaburi tunakohifadhia ndugu zetu, barabara imekatika na kuleta changamoto hivyo inafika wakati magari hayawezi kufika kule chini, hivyo nitakapokuwa Diwani nitashughulikia suala hilo,” ameeleza Regina.
Aidha, amewaomba wananchi wa Pasiansi kuwapigia kura wagombea wote wa CCM akiwemo yeye, na baada ya uchaguzi wawadai maendeleo kwa pamoja.

Amesema atashirikiana na wananchi kuhakikisha Kata ya Pasiansi inapata maendeleo endelevu.
“Pasiansi mpya itajengwa na mimi na wewe. Nikipata ridhaa ya kuwa Diwani nitashirikiana na ninyi wananchi kuleta maendeleo na kupata Pasiansi mpya na iliyo njema,” amesema Regina.

Pamoja na hayo, ameahidi kufuatilia suala la upimaji shirikishi uliofanyika mtaa wa Pasiansi Juu, ambapo wananchi hawajapatiwa hati za umiliki hadi sasa, na kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wa mtaa wa Bwiru Elimu.
Kwa upande wake, mkazi wa Pasiansi Juu, Chacha Mares amesema sera na maono ya mgombea huyo ni mazuri na kwamba endapo atayatekeleza kama alivyoahidi, kata hiyo itapiga hatua kubwa kimaendeleo.


