Na Saada Almasi – Simiyu.
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Gesi ya Oryx imetoa mitungi 300 pamoja na vifaa vyake kwa watumishi wa jeshi la magereza mkoani Simiyu ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kitaifa ya kuachana na matumizi ya nishati chafu ifikapo mwaka 2034.
Ugawaji wa mitungi katika magereza hayo ni kati ya magereza 129 na taasisi zake yaliyopangwa kufikiwa na wakala huyo kwa nchi nzima ambapo kwa mkoa wa Simiyu tayari askari wa jeshi hilo wapatao 300 wamekabidhiwa lengo likiwa ni kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Akipokea mitungi hiyo mkuu wa jeshi la magereza Mkoani Simiyu, Lugano Msomba amesema kuwa tangu mwezi Disemba 2024 Jeshi la Polisi mkoani humo tayari limekwisha achana na matumizi ya nishati chafu hivyo mitungi hiyo kwa watumishi inakwenda kuendelea kudhibiti matumizi ya nishati chafu.

“Jeshi la Magereza tumeacha kutumia nishati chafu tangu mwaka jana lakini watumishi baadhi yao bado hawakuwa na nishati safi huu ni muda mzuri niwashukuru REA kwa kuona umuhimu wa kutoa kwa watumishi wetu,” amesema Kamanda Msomba.
Akizungumza wakati wa utoaji wa mitungi hiyo Mjumbe wa Bodi ya REA, Lucas Malunde amesema kuwa makubaliano ya wakala huyo na jeshi la magereza nchini ni kuwapatia majiko na mitungi elfu kumi na tano na kuwataka waendelee kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati salama.

“Kama kauli mbiu yetu ya REA inavyosema kwamba okoa Maisha tunza mazingira tunategemea tunakwenda kuokoa Maisha ya watumiaji wa nishati chafu baada ya kuhamia katika nishati safi na kuokoa mazingira lakini pia tutakuwa tunatekeleza kwa viteno makubaliano yetu na jeshi la magereza la kuokoa mazingira”amesema Lucas.
Naye Msimamizi wa wa Kampuni ya Oryx Mkoa wa Simiyu, Gibson Rogers akitoa maelekezo juu ya nama ya kujikinga na madhara ya moto wa gesi amesema kuwa yafaa kuchukua tahadhari za matumizi ya gesi kwa kuhakikisha gesi na jiko vimekaa umbali unaotakiwa lakini pale viashiria vya kuvuja kwa gesi vinaposikika basi ni vema kufungua milango na madirisha kisha kutoa mtungi unaovuja nje.

“ikatokea moto umelipuka katika mtungi lazima ujue ni moto mkubwa au mdogo kama ni mkubwa omba msaada jeshi la zimamoto na uokoaji lakini kama ni mdogo loweka taulo kwenye maji kisha zungusha kwenye mtungi pale panapo waka hapo utakuwa umezuwia hewa ya oxygen kupita hivyo moto utazimika,muhimu usitumie maji kwani yana oxygen inayoongeza kasi ya moto,” ameeleza Gibson.
Jumla ya magereza 129 na taasisi zake nchi nzima yanakwenda kunufaishwa na huduma hizo zenye gharama ya shilingi Bilioni 35 ambapo unaohusisha ujenzi wa miundombinu ya biogas, upelekaji wa gesi asilia katika gereza la Ilungu mkoani Lindi ,usambazaji wa mkaa mbadala na mashine za kutengenezea mkaa ambazo ni 61 kwa magereza mbalimbali nchini sambamba na kuwapa mafunzo watumishi 280, namna ya kutumia nishati hizo


