REA WAFIKISHA ‘MWANGAZA’ WA MAISHA, KIUCHUMI MWANUBI

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Katika kuendeleza huduma za usambazaji umeme hususani katika maeneo ya vijini serikali kupitia  wakala wa nishati vijijibi REA  imewasha umeme katika kitongoji cha Mwanumbi kijiji cha Kolandoto kata ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga  lengo likiwa ni  kuhakikisha vijiji na vitongoji nchini vinafikishiwa huduma  hiyo  ambayo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi.

Hafla ya uwashaji umeme huo imehudhuriwa na waziri wa Nishati,   leo, Agosti 10, 2026, ambapo amesema   umeme ni hitaji la msingi kwa Watanzania na nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuanisha kuwa  Serikali inaendelea kupanua miundombinu ya umeme vijijini na vitongojini ili kuwawezesha wananchi kutumia nishati hiyo katika shughuli za uzalishaji na kuboresha maisha yao.

Amesema kufikishwa kwa umeme kunapaswa kwenda sambamba na matumizi yenye tija, ikiwemo kuongeza thamani ya mazao, kukuza biashara, kuanzisha shughuli za uzalishaji na kuongeza kipato cha wananchi.

“Umeme siyo tu kwa ajili ya kuwasha taa, bali ni kichocheo cha uzalishaji na maendeleo. Wananchi wanapaswa kutumia fursa hii kuongeza thamani ya mazao, kukuza biashara na kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi,” amesema Ndenjembi.

Aidha waziri Ndejembi  amewahimiza wananchi ambao miundombinu ya umeme imefika katika maeneo yao kuchangamkia fursa hiyo kwa kuunganishiwa huduma kwa gharama ya Shilingi 27,000 na kuitumia katika shughuli zitakazowaongezea kipato.

Lakini pia  ameiagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufanya tathmini ya maeneo ambayo bado hayajafikiwa na miundombinu ya umeme ili yaingizwe katika mipango ya utekelezaji na kufikishiwa huduma hiyo  na kuwataka  wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme kuongeza kasi ya usimikaji wa nguzo na ujenzi wa miundombinu katika maeneo yaliyosalia ili wananchi wengi zaidi waweze kufikiwa na kuunganishiwa huduma.

Amesisitiza kuwa shule, zahanati na maeneo mengine ya huduma za kijamii yanapaswa kupewa kipaumbele katika kufikishiwa umeme kutokana na umuhimu wake katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuanisha kwamba  Serikali  inaendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika na kufungua fursa za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,  Mboni Mhita, ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote vya Mkoa wa Shinyanga, akisema hatua hiyo imefungua fursa mpya za maendeleo kwa wananchi na kwamba  upatikanaji wa umeme vijijini umechangia kuboresha shughuli za kiuchumi, uzalishaji, ajira na huduma za kijamii, huku akieleza kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha vitongoji vilivyosalia vinafikiwa na huduma hiyo.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA,  Herini Mhina, amesema Wakala unaendelea kutekeleza miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji mbalimbali nchini ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi, hususan walioko maeneo ya vijijini, wanapata huduma hiyo na kusema kuwa  REA itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kupanua wigo wa upatikanaji wa umeme na kuwawezesha wananchi kutumia nishati hiyo katika shughuli za kiuchumi, uzalishaji na utoaji wa huduma za kijamii.

Diwani wa Kata ya Kolandoto, Mshagatila Moses, amesema anawashukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwafikishia wananchi wa Kitongoji cha Mwanubi huduma ya umeme, akieleza kuwa nishati hiyo itachochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa upande wao Wananchi wa Kitongoji cha Mwanubi akiwemo Agines Machiya mkazi wa Mwanubi na Yohana Mabula mwenyekiti wa kijiji cha Kolandoto  wameishukuru Serikali kwa kuwafikishia huduma ya umeme, wakisema hatua hiyo itafungua fursa mpya za biashara na uzalishaji pamoja na kuongeza thamani ya mazao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *