RC TABORA CHACHA ASIKITISHWA NA MTUHUMIWA KESI YA ULAWITI KUACHIWA HURU.

Na, PASCAL TULIANO, Tabora.

Mkuu wa mkoa wa Tabora Paul, Matiko Chacha amesikitishwa na kitendo Cha kuachiwa huru mtuhumiwa wa kesi ya ulawiti kwa mtoto wa kiume wa darasa la pili mkoani humo.

Paul Chacha amesema mtuhumiwa huyo baada ya kukutwa na hatia alifungwa kifungo Cha miaka 30 jela, lakini cha kushangaza aliachiwa huru huku bibi wa Mtoto huyo akiendelea kumuuguza mtoto katika hospitali ya taifa ya Muhimbili.

Mkuu huyo wa mkoa wa Tabora ameonyesha masikitiko hayo wakati akizungumza na viongozi wa serikali, viongozi wa dini na kamati ya ulinzi mkoani humo, ambapo amesema kitendo hicho kinakatisha tamaa katika harakati za kuitetea jamii dhidi ya vitendo hivyo.

“Hapa Tabora tumekamata watu wasiopungua watano, mtoto mdogo mvulana wa darasa la Tano amefanywa vibaya sana, mpaka Leo anahudhuria matibabu Muhimbili, yule mtuhumiwa alihukimiwa miaka 30, lakini ameachiwa huru. Nimemuuliza mwanasheria wetu anasema ‘hakimu alisema tumeshindwa ‘technicality’. Hivi wewe hakimu unayeruhusu hilo hauna mtoto kweli?. Haya mambo Mimi sioni aibu kuyakemea.” – RC Chacha.

Jambo FM imezungumza na wananchi wa Tabora ambapo wameonyeshwa kusikitisha na matukio ya ulawiti huku wakitoa maoni juu ya nini kinapaswa kufanyika.

Mama Zoma amesema “Kutokana na haya mambo Mimi naomba wenyeviti wa mitaa waweke utaratibu wa kuitisha vikao walau mara Moja kwa mwezi ili kupeana elimu na kukemea haya mambo katika jamii zetu, na wazazi ambao watoto wao wanafanyiwa hivyo wawe wepesi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa katika vyombo vya Dola hata kama aliyefanya ni ndugu yako.”

Jamal Chambogo anasema “Mimi naona vijana wapewe elimu maana vijana ndiyo wahanga wakubwa, lakini wazazi wawe makini sana na familia zao maana haya mambo yanatisha sana.”

Mwisho mkuu wa mkoa Paul Chacha ameapa kupambana na taasisi zinazohusika kueneza uovu huo kwa jamii hasa watoto wadogo.

“Hizo taasisi sio kwamba hazipo, nilipoteuliwa na Rais kuja hapa Tabora niliapa kabla sijafika hapa hayo mashirika nisiyakute ilimradi taasisi yako imetajwa, potelea mbali ila Mungu ataona nilikuwa na nia njema.” Amesema RC Chacha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *