Afarah suleiman, Babati – Manyara.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ametembelea Gereza la Wilaya ya Babati na kukagua utekelezaji wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Solomoni Mwambingu na Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Manyara wamesema hadi kufikia mwaka jana Desemba 2024 waliweza kutekeleza maagizo ya Serikali kwa asilimia 100 na Magereza yote katika Mkoa wa Manyara yanatumia Nishati safi ya kupikia.
Baada ya kupokea taarifa hiyo na kufanya ukaguzi na kuona namna mitambo ya nishati safi inavyofanya kazi, RC Sendiga amewapongeza Jeshi la Magereza Manyara kwa utekelezaji huo wa maagizo ya Serikali kikamilifu.
Aidha, RC Sendiga ametumia nafasi hiyo kuendelea kuwasisitiza Wananchi, Taasisi za Umma na binafsi katika Mkoa wa Manyara kutumia nishati safi, ili kulinda afya zao dhidi na moshi unaotokana na matumizi ya Nishati zisizo safi na salama kwa binadamu, ikiwemo kuni na mkaa.