Na Clavery Christian – Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amewataka Maafisa Usafirishaji wakiwemo Madereva Boda boda, bajaji na Guta kujirasimisha kwenye mamlaka za urasimishaji, ili kutengeneza mazingira ya kupata mikopo kutoka kwenye taasisi mbalimbali za fedha na kuwawezesha kukua zaidi kibiashara.
RC Mwassa ameyasema hayo kwenye Kongamano la Wafanyabiashara wadogowadogo, Wajasiriamali na Maafisa Usafirishaji wa Bukoba Mjini, Mkoani Kagera ambapo alisema kiu yake ni kuona maafisa usafirishaji wanamiliki vyombo wanavyoviendesha wao wenyewe.
“Mimi fahari yangu kubwa ni kuona maafisa usafirishaji wote mnamiliki wenyewe pikipiki mnazoziendesha,” alisema Mwassa.
Ameongeza kuwa, ushirikiano kati ya Maafisa usafirishaji na mamlaka za usalama barabarani unazidi kuimarika na jitihada zinaendelea kufanyika kuhakikisha wanafanya kazi yao kwa amani bila shida.

Mwassa amesema Serikali imeendelea kutoa fursa za ajira zisizo rasmi kwa vijana kupitia miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa Kagera ambapo ni pamoja na ujenzi wa barabara, bandari na mradi wa bomba la mafuta ghafi unaopita katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Kagera.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na taasisi kama VETA, ili kuwapatia vijana mafunzo ya ufundi stadi yanayowasaidia kupata ajira na kipato, sambamba na kuwawezesha kuwa wabunifu katika kubuni vyanzo mbalimbali vya kujitegemea.
Alisema kuwa Serikali itaendelea kutoa msaada wa vifaa muhimu kwa ili kuimarisha kongani ya vijana, huku akitoa wito kwa vijana kufanya kazi kwa bidii bila kujihusisha na makundi yasiyokuwa na tija kwa maendeleo yao.


