RC MWASA AIFAGILIA HALMASHAURI YA BUKOBA KWA KUPATA HATI SAFI, KUVUKA LENGO LA MAKUSANYO

Na Clavery Christian -Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwasa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kwa Kupata hati safi na kuvuka lengo la makusanyo ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2024/25 kutoka shilingi Bilioni 3.1 hadi Bilioni 3.4 sawa na asilimia 112 hadi kufikia Mei 31,2025.

Hayo yamesemwa katika kikao maalum cha baraza la madiwani la kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Serikali (CAG) kilichofanyika katika ukumbi wa Chemba.

“Mheshimiwa Mwenyekiti natambua kuwa halmashauri yako katika ukaguzi wa hesabu sa serikali 2023/24 imepata hati safi,niwapongeze sana kwa jitihada zenu ambazo zimeisaidia Halmashauri yenu kupata hati safi,” alisema Mwasa.

Alisisitiza kufanikiwa kupata hati safi siyo rahisi lakini kuendelea kushikilia nafasi hiyo ni kazi kubwa, hivyo aliwaelekeza waheshimiwa madiwani, mkurugenzi mtendaji na watumishi kujikita kikamilifu katika kusimamia sheria, taratibu na miongozo ya serikali ili kuendelea kupata hati safi na kupata fedha za maendeleo.

RC Mwasa aliongeza kuwa vigezo vinavyotumika katika upimaji wa utendaji kazi wa halmashauri ni pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani, ambayo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ni ya kuridhisha kwani kufikia Mei 31,2025 Halmashauri imeshavuka lengo la makusanyo ya mwaka huu wa fedha.

Katika hitimisho la hotuba yake RC Mwasa aliwataka watumishi kuzingatia matumizi ya mfumo wa ukusanyaji fedha yani TAUSI, huku akiitaka halmashauri kuhakikisha inakusanya mapato yatokanayo na ushuru wa mabango na kodi za majengo

Akitoa shukrani kwa niaba ya baraza la madiwani, Diwani wa kata ya Kaibanja Mheshuimiwa. Jason Rwankomezi alimshukuru RC Mwasa kwa kufika kwenye baraza la hoja za CAG na kuleta  habari njema ya Halmashauri kupata hati safi huku akiahidi ushirikiano zaidi kutoka kwenye baraza la madiwani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *