
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka watumishi wa Sekta ya ardhi wa mkoa huo kua na utaratibu wa kufanya tathmini katika kazi zao ili kuweza kubaini mapungufu waliyonayo na kuyarekebisaha.

Mtanda ameyasema hayo hii leo wakati akifungua kikao cha Watumishi wa Sekta ya Ardhi Mkoa wa Mwanza na ambapo ameipongeza sekta hiyo kwa kazi kubwa ambayo imekua ikifanya huku akiwataka kujenga utaratibu kwa kufanya tathmini za kazi zao kwani hii itasaidia kutambua ni kipi wamekosea na kujirekebisha ili waweze kufikia malengo.
“Mtu yoyote anayependa maendeleo lazima ajifanyie tathmini ya mwaka mzima, ni watu wachache wanaopenda kufanya tathmini, unapojitathmini utajua wapi pa kurekebisha”.
Katika hatua nyingine Mtanda pia amewataka watumishi hao kuwatumia wataalamu wa sekta nyingine pale wanapotaka kufanya tathmini hizo ili waweze kuwapa mawazo mapya na chanya ambayo yatawajenga zaidi.
“Mnaweza kukaa humu ndani mkajifungia mkaongea na mpaka muda wa chakula ukafika mkala lakini kumbe mnafanya tathmini ya uongo, sasa ni lazima muambiane ukweli” Amesema Mkuu wa Mkoa.

Aidha pia amewataka Wataalamu wa Ardhi kufanya kazi kwa weledi huku wakishughulikia migogoro ya ardhi kwa ufasaha kwani itasaidia kupunguza migogoro mingine ambayo inaweza kujitokeza.
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo kwa Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Mwanza kuhakikisha kunakuwepo na operesheni za Wilaya kwa Wilaya kuhusu kliniki za ardhi walau mara mbili kwa mwaka.
Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza Bw. Wilson Lugi amesema wamekutana kama wataalam kufanya tathmini ya kiutendaji ya mwaka 2024/2025 na kupanga namna ya kufanya vyema 2025/26.
Kamishna huyo wa Ardhi Msaidizi amesema wametekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kutoa hati, usimamizi na utekelezaji wa miradi mbalimbali, Pia wamefanikiwa kukusanya maduhuli ya Serikali zaidi ya sh. bilioni 8.7 sawa na 42% ya makusudio.