Na Daniel Gahu – Katavi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amewataka maafisa ugani mkoani humo kuweka malengo mahsusi na yanayopimika ya tija kwa kila zao linalozalishwa, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, ufanisi wa kilimo na ushindani wa mazao ya Katavi katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
RC Mrindoko ametoa agizo hilo baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea mabanda 15 ya Mkoa wa Katavi katika Maonesho ya Nanenane, ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji, ubunifu na teknolojia zinazotumika katika sekta ya kilimo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mrindoko amesema maafisa ugani wanapaswa kuacha mtazamo wa kutoa elimu pekee na badala yake kuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha maarifa wanayowapatia wakulima yanatafsirika kuwa ongezeko la uzalishaji, kipato na ushindani wa mazao katika masoko.
“Tunapaswa kuweka malengo ya tija kwa kila zao tunalolima ili tujue tunazalisha kiasi gani, tunahitaji kuongeza wapi na namna gani tunaweza kufikia ushindani wa soko. Maafisa ugani msiishie kutoa elimu pekee, bali muwe chachu ya mabadiliko katika kuongeza uzalishaji wa wakulima,” amesema Mrindoko.

Amesema kuwepo kwa malengo yanayopimika kutasaidia wataalamu wa kilimo kutambua kiwango halisi cha uzalishaji wa kila zao, kubaini changamoto zinazowakabili wakulima na kuweka mikakati ya kuongeza tija kwa kuzingatia mahitaji ya soko.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka maafisa ugani kutumia Maonesho ya Nanenane na majukwaa mengine ya kitaalamu kama fursa ya kujifunza mbinu na teknolojia mpya zinazoweza kuongeza tija katika kilimo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wataalamu wa kilimo kufanya tafiti kuhusu mazao mapya yanayoweza kustawi katika mazingira ya Katavi, akitolea mfano wa parachichi na chia, ambayo amesema yanaweza kuwa sehemu ya kuongeza wigo wa uzalishaji na fursa za kiuchumi kwa wananchi.
“Ni muhimu wataalamu wetu kuangalia mazao mengine ambayo yanaweza kustawi hapa Katavi. Tafiti zifanyike ili tujue ni mazao gani mapya yanaweza kuleta tija na kuongeza kipato kwa wananchi,” amesema.

Mrindoko pia amezitaka taasisi zote mkoani Katavi kutenga bajeti kwa ajili ya kuwawezesha maafisa ugani kushiriki katika mafunzo, warsha na matukio mbalimbali ya kitaalamu yatakayowaongezea maarifa na uwezo wa kuwahudumia wakulima kwa ufanisi zaidi.
Ametaja pia Wiki ya Mwanakatavi, inayotarajiwa kufanyika Oktoba 2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, kuwa ni miongoni mwa majukwaa muhimu ambayo maafisa ugani wanapaswa kushiriki, akieleza kuwa matukio ya aina hiyo hutoa fursa ya kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya, kuongeza ubunifu na kuchochea ari ya utendaji kazi.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha wakulima kuhusu upimaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Katavi, akieleza kuwa taarifa sahihi kuhusu aina na uwezo wa ardhi zitawasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi ya kilimo na kuongeza tija.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha kilimo mkoani Katavi kinabadilika kutoka kilimo cha mazoea kwenda kilimo chenye tija, kinachozingatia takwimu, teknolojia, mahitaji ya soko na kuongeza kipato cha mkulima.

Kwa msisitizo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wataalamu wa kilimo na maafisa ugani kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matokeo, akibainisha kuwa mafanikio ya sekta ya kilimo yanapaswa kupimwa kupitia ongezeko la uzalishaji, kipato cha mkulima na uwezo wa mazao ya Katavi kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.


