Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita ameendelea na ziara yake ya kujitambulisha rasimi katika halimashuri zote sita za mkoa huo,ambapo amefanya kikao kazi na watumishi wa Manispaa ya Shinyanga na kusisistiza udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato, uwajibikaji, uadilifu na utatuzi wa changamoto za wananchi.
RC Mboni amefanya kikao chake hicho katika ukumbi wa kalinjuna uliopo katika katika halimashuri ya manispaa ya Shinyanga na kuwataka Wakuu wa Idara na Vitengo kuhakikisha wanasikiliza na kushughulikia kero za wananchi kwa wakati.

“Si jambo la busara kuona wananchi wanalalamika kuhusu huduma wakati ninyi mpo kazini. Wananchi wanahitaji huduma bora, na ninyi ndio mnapaswa kuwa suluhisho,” amesema mboni.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuhakikisha mianya ya upotevu wa mapato inazibwa, huku pia akielekeza jitihada za kuongeza vyanzo vipya vya mapato kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya manispaa hiyo.

“Kila senti inayokusanywa itumike ipasavyo. Tengeni maeneo kwa ajili ya wawekezaji ili kukuza uchumi wa manispaa na kuongeza ajira kwa wananchi wetu,” ameongeza Mboni.
Lakini pia RC Mboni amesema miradi yote ya kimkakati ambayo haijakamilika inapaswa kupewa kipaumbele katika utekelezaji na usimamizi wake, ili iweze kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Katika hatua nyingine, RC Mboni ameendelea kutoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika kushiriki uchaguzi mkuu ujao, akisema hiyo ni sehemu muhimu ya kukuza demokrasia na kuwapa wananchi nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Mwl. Alexcious Kagunze amempongeza RC Mboni kwa kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa huo, na kuhaidi kutekeleza maagizo yote kwa weledi, ikiwemo kusimamia mapato, uwekezaji, miradi ya maendeleo na maandalizi ya uchaguzi.


