RC MHITA ATAKA KASI UKAMILISHWAJI JENGO LA MAMA NA MTOTO KAHAMA

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita ametembelea ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Manispaa ya  Kahama na kuagiza kuongezwa kasi ya ujenzi, ili kukamilisha mradi kwa wakati.

Akizungumza mara baada ya kukagua hatua za utekelezaji wa mradi, RC Mboni amesema ujenzi huo ni wa kimkakati kwa mkoa wa Shinyanga, wenye lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto, hivyo kasi ya ujenzi ni lazima iendane na thamani ya fedha.

“Kasi ya ujenzi iongezeke, Suma JKT ambao ndio wakandarasi wa mradi huu muongeze bidii ili jengo likamilike mapema. Fedha inayowekwa ni nyingi, ni lazima ionekane kwenye hatua za ujenzi,” amesema  RC Mboni.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu amesema fedha za kumalizia ujenzi huo zipo, lakini zitatolewa kulingana na kasi na ubora wa kazi unaoendana na fedha zilizolipwa awali.

Naye, Mhandisi wa mradi huo  kutoka SUMA JKT,  James Simon amesema wapo tayari kuongeza kasi, ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa wa Januari 2026 kama mkataba unavyobainisha.

Mradi huo, unatekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani ambapo tayari kiasi cha Shilingi Bilioni 2.7 kimelipwa na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 75 badala ya asilimia 80 iliyotarajiwa kufikiwa kwa hatua ya sasa.

Mpaka kukamilika kwa jengo hilo zaidi ya bilioni 6.8 zitatumika na linatazamiwa kuwa mkombozi wa kupunguza vifo vya Mama na Mtoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *