RC MBONI MHITA ATEMBELEA MAONYESHO YA SABASABA.

NA EUNICE KANUMBA 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita,  amesema kuwa Mkoa wa Shinyanga unaendelea kwa kasi kubwa kutekeleza kwa vitendo maelekezo, maono na dhamira ya Dr Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo jumuishi kwa wananchi wote kupitia miradi ya kimkakati na uwekezaji wa kisasa.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu  Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam,  Mboni ameeleza  kuwa Mkoa wa Shinyanga umejipanga vizuri kuendeleza juhudi za Serikali kwa kuwekeza katika maeneo ya vipaumbele vilivyoainishwa na Mheshimiwa Rais.

Amesisitiza  kuwa Mkoa huo sasa unalenga kujitofautisha kiuchumi kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo kuongeza uzalishaji wa zao la Pamba, kwa kuliongezea thamani, Kongani Maalum ya Uwekezaji ya Buzwagi (Buzwagi Special Economic Zone – SEZ) iliyopo Manispaa ya Kahama.

“Kwa heshima kubwa tunampongeza na kumshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kuijenga Tanzania ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara. Mkoa wa Shinyanga tumejipanga vyema kuhakikisha tunasimamia utekelezaji wa dira hiyo kwa matendo yanayoonekana. Tunataka Shinyanga iwe mfano wa mafanikio ya dhana ya maendeleo kwa vitendo,” amesema  Mboni.

Akiwa ameambatana na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo  RC. Mboni ametumia  fursa hiyo kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bi. Latifa Khamis, ambapo walijadili namna bora ya kuimarisha ushiriki wa Mikoa katika maonesho hayo na kuongeza fursa za biashara na uwekezaji.

Kwa upande wake,  Latifa Khamis amempongez  RC. Mboni kwa uteuzi wake na kuaminiwa na Mheshimiwa Rais, sambamba na juhudi zake za kuhakikisha Mkoa wa Shinyanga unashiriki kikamilifu katika maonesho haya ya kimataifa ambayo ni jukwaa muhimu la kukuza biashara, uhusiano wa kibiashara na usambazaji wa maarifa kati ya wadau mbalimbali wa sekta ya uchumi.

Aidha,RC  Mboni amewapongeza  wataalam wa Mkoa huo kwa namna walivyojipanga kushiriki maonesho hayo, huku akimpongeza kipekee Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Shinyanga,  Margareth Warioba, kwa uongozi wake mahiri uliowezesha timu ya Mkoa pamoja na wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo,ambapo ameanisha kuwa   kupitia ushiriki huo, Mkoa wa Shinyanga umetangaza bidhaa zake, vivutio vyake vya uwekezaji na uwezo wake wa kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta binafsi na ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *