RC Macha:NGO’S Zichochee Maendeleo Shinyanga

Na Eunice Kanumba,Shinyanga

Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Shinyanga yametakiwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kutatua changomoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, kwa lengo la kuchochea maendeleo pamoja na kuzalisha ajira zaidi hususani katika kilimo,mifugo na uvuvi.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Shinyanga uliofanyika Agosti 28,2024 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo amezitaka kuendelea kupambana na ukatili dhidi ya watoto, wanawake na watu wenye ulemavu huku akiainisha kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa kwa sasa likichangiwa zaidi na suala la ukosefu wa malezi hasa kwa vijana.

“Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya jamii, na tutaendelea kushirikiana nanyi hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha kwamba mnatekeleza wajibu wenu kwa kuzingatia sheria na utamaduni wa nchi yetu,” amesema RC Macha.

Aidha, amewapongeza viongozi wa mashirika hayo kwa kuajiri vijana na kuchangia kupunguza tatizo la ajira nchini huku akisisitiza umuhimu wa ajira hizo kutolewa kwa haki na kuzingatia vigezo vya kitaaluma badala ya upendeleo wa kifamilia.

Katika hatua nyingine RC Macha ameyataka mashirika hayo kutokuingilia mamlaka za utawala za maeneo wanayofanyia kazi na badala yake kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wa maeneo husika ili kufanikisha utekelezaji wa miradi yao kwa ufanisi zaidi.

Awali akisoma risala mbele ya Mkuu wa Mkoa Mwenyekiti wa Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Shinyanga Bakari Kibile amesema mashirika hayo yamekuwa ni kiungo muhimu katika mkoa huo hususani katika suala la kulinda haki za binadamu kwa kushirikiana na idara mbalimbali za serikali na kuiomba serikali kutoa vibali vya utekelezaji wa miradi kwa wakati ili jamii inufaike na uwepo wa mashirika hayo.

Pia Kibile amebainisha kuwa mashirika yote 116 yaliyosajiliwa mkoani Shinyanga yanaendelea kutoa huduma muhimu kwa jamii, ikiwemo elimu, afya, haki za binadamu, na ujasiriamali na kubainisha kwamba yamekuwa na mchango mkubwa katika kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake, huku akiomba serikali kuendelea kuboresha mazingira ya utekelezaji wa miradi yao kwa kutoa vibali kwa wakati na kuhamasisha mahusiano mazuri kati ya serikali na mashirika hayo.

Nao Washiriki wa mkutano huo wameishukuru serikali kwa ushirikiano wanaoupata na kuomba kuwepo kwa miradi ya ndani ili kupunguza utegemezi wa miradi inayofadhiliwa kutoka nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *