![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2024/09/MACHA.jpeg)
Na Eunice Kanumba,Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mh. Anamringi Macha amewasihi wananchi mkoani wa Shinyanga kujitokeza na kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la Uandikishaji wa Wapiga kura linalotarajiwa kuanza Septemba 11 hadi Oktoba 20,2024 ili kuweza kuchagua viongozi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
RC Macha ameyasema hayo Septemba 5,2024 wakati akihutubia wajumbe wa Kikao cha Wadau wa Mpango wa matumizi ya ardhi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga ambapo ia amewataka wananchi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo
“Niwaombe sana Wanashinyanga, tujitokeze kwa umoja wetu na kila mwenye sifa ya kujiandikisha kupiga kura aende katika maeneo yetu tunayoishi kuanzia tarehe 11 hadi 20 Oktoba, 2024 ili itakapofika wakati wa kuchagua viongozi aweze kutumia vema haki yake hiyo ya msingi,” amesema RC Macha
Aidha, RC Macha amesema kuwa baada ya kujiandikisha mwananchi anayo haki ya kugombea nafasi hizo za uongozi kupitia vyama vya siasa na baadae kutafuatiwa na zoezi la Upigaji wa kura kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa ifikapo t Novemba 27 mwaka huu.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2024/09/DC.jpeg)
Katika hatua nyingine RC Macha amewataka wajumbe wote waliohudhuria kikao hicho kwenda kuwa mabalozi na kusaidia kutoa elimu kwa wananchi, na wale wote wanaowazunguka katika maeneo yao ili waweze kushiriki vema katika zoezi hilo linalokuja huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa matangazo ili kuwakumbusha wananchi kushiriki kikamilifu wakati ukifika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 27,mwaka huu nchini kote ambapo viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji watachaguliwa kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ambapo kwa Mkoa wa Shinyanga jumla ya Mitaa 90, Vijiji 506 na Vitongoji 2749 vinatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2024/09/WAJUMBE-3.jpeg)