Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amewatoa hofu Watumishi wa Serikali juu ya suala la Kikokotoo,akieleza kwamba Rais Samia ni msikivu na atalifanyia kazi suala hilo
Amebainisha hayo leo Mei 1,2024 kwenye Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) mkoani Shinyanga yaliyofanyika Kata ya Kakola wilayani Kahama ambapo amesema suala la Kikokotoo limesemwa vya kutosha kila mahali hadi kufikishwa Bungeni, na kwamba anaimani Serikali imelisikia na italifanyia kazi kwa maslahi ya wafanyakazi nchini.
Katika hatua nyingine RC Macha amewataka Waajiri wa Sekta binafsi kupeleka Michango ya Watumishi wao kwenye Mifuko ya hifadhi ya jamii suala ambalo limekuwa likilalamikiwa na Watumishi mara kwa mara na hata kuleta Migogoro kwenye ulipwaji wa mafao akiwasisitiza kuzingatia Sheria za ajira kwa watumishi wao,pamoja na kuwapatia Mikataba mizuri isiyo andamizi,huku akiwasihi Watumishi nao kutokubali kupewa Mikataba Mibovu.
Pia ametoa rai kwa watumishi wa Serikali hususani walimu,watumishi wa afya na Kilimo kutojiingiza kwenye Mikopo Kausha damu ambayo imekuwa ikiwadumaza Kimaendeleo na kuwaahidi watumishi wa Serikali kwamba yale yote ambayo wamewasilisha kwenye Risala yao yanayogusa ngazi ya Kitaifa likiwamo pia suala la Kikokotoo na Vifurishi vya Bima ya Afya atayafikisha sehemu husika kwa maandishi.
Akizungumza kwenye Maadhimisho hayo,Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Shinyanga Mathias Balele amesema Kilio kikubwa cha Wafanyakazi ni Kikokotoo na kubainisha kwamba tatizo la Kikokotoo ni kanuni na siyo Sheria.
Awali Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Shinyanga Ramadhani Mpangala,kupitia risala aliyoisoma katika maadhimisho hayo amesema Changamoto kubwa ambayo inawakabili wafanyakazi ni suala la Kikokotoo ambalo limekuwa Kaa la Moto kwa wafanyakazi na kumuomba Rais Samia aliangalie upya.
Ametaja Changamoto nyingine kuwa ni ucheleweshwaji malipo ya mafao kwa wastaafu na waajiri hasa wa sekta binafsi kutopeleka michango ya watumishi katika Mifuko ya hifadhi ya jamii,pamoja na waajiri kutoruhusu Watumishi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi.