Na Eunice Kanumba –Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amewataka wananchi kulipa Ankara za maji kwa wakati, ili kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama inaendelea kusambaza katika maeneo ya mkoa huo na kuwatahadharisha wenye nia ovu ya kujipatia huduma ya maji kwa njia isiyo halali kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.
RC Macha ameyasema hayo leo Aprili 14, 2025 alipokuwa akiongea na watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) ambao walifika katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwenye hafla ya kukabidhi Magari mawili (2) mapya yenye thamani ya takribani Milioni 276 yenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka hiyi SHUWASA.

“Serikali haipo tayari kabisa kumtetea mtu yeyote na wala haitakuwa na muhali kwa mwananchi yeyote mwenye nia ovu ya kujipatia huduma ya maji kwa njia isiyokuwa halali, na badala yake itamchukulia hatua za kisheria ikiwemo kumfikisha Mahakamani ili iwe mfano kwa yeyote asiyeitakia mama Mamlaka,” amesema RC Macha.
RC Macha pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza Menejimenti ya SHUWASA inayoongozwa na Mhandisi Yusuph Katopola na watumishi wote kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa asilimia 95 Mjini na 85 kwa maeneo ya Vijijini huku pongezi zaidi ni kwa utekelezaji wa mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Shinyanga na Miji inayokuwa kwa kasi ikiwemo Tinde, Didia na Iselamagazi huku ikitajwa takribani Bilioni 231 zinatarajiwa kutumika katika mradi huo.

SHUWASA inatekeleza Mradi huo wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga wenye zaidi ya Bilioni 231 unajumuisha sehemu kuu tatu (3) yaani Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Majisafi, Ujenzi wa Miundombinu ya Usafi wa Mazingira na Kuimarisha Uwezo wa Taasisi ambapo sasa imeweza kununua magari mawili (2) yanye thamani ya takribani Mil 276 Shilingi za Kitanzania magari ambayo yatawezesha ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya utekelezaji wa mradi na kuongeza ufanisi wenye kufanikisha malengo kwa wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa SHUWASA Yusuph Katopola amekiri kupokea malekezo na ushauri wa RC Macha huku akiongeza kwa kusema kuwa Magari hayo yanakwenda kuongeza usimamizi, ufuatiliaji na ufanisi wa mradi lengo likiwa ni kuhakikisha huduma ya maji inafikia 98% baada ya kukamilika kwa mradi.


