Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

RC Macha Ahimiza Matumizi ya Fursa Hii Kwa Wajasiriamali Shinyanga

Na Eunice Kanumba,Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamiringi Macha amewataka wajasiriamali wanaotengeneza bidhaa za ngozi katika mkoa wa Shinyanga kutumia vizuri fursa za upatikanaji wa ngozi kutokana na machinjio ya wanyama yaliyopo halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga   kutengeneza bidhaa nyingi zaidi na hivyo kukuza uchumi wa Taifa.

RC Macha ameyasema hayo Septemba 9,2024 wakati akifungua mafunzo ya wajasiriamali wanaotengeneza bidhaa za ngozi Manispaa ya Shinyanga ambayo yanaratibiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambayo  yanafanyika kwa  muda wa siku (2) kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kuhudhuriwa na wataalam mbalimbali kutoka TAMISEMI, SIDO, TBS, na wadau wengine   huku akisisitiza ubunifu zaidi.

“Ningependa kuwaasa mjitahidi kutumia vizuri fursa za upatikanji wa ngozi kwa sababu ndani ya Mkoa wa Shinyanga kuna machinjio ya wanyama mbalimbali kama ng’ombe, mbuzi na kondoo ambayo kupitia machinjio haya mnaweza mkapata kiasi kikubwa cha ngozi na mkafanikiwa kutengeneza bidhaa nyingi zaidi na kupata faida kubwa hatimaye kukuza uchumi wetu na Serikali na kuongeza pato la taifa ” amesema RC Macha.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kitengo cha Tafiti na Mafunzo, Mwalimu Hamisi Mwanasala amesema mafunzo hayo yamelenga kuwafikia wajasiriamali takribani 40 wanaojishughulisha na bidhaa za ngozi na amewataka washiriki wote kutumia vema mafunzo haya ili kuboresha bidhaa wanazozalisha ziendane na viwango vya TBS.

“Mafunzo haya yamekusudia kuwasaidia wajasiriamali wanaojishughulisha na bidhaa za ngozi takribani 40 ili waweze kuboresha  bidhaa zao za ngozi ziendane na viwango ambavyo Shirika la Viwango Tanzania limethibitisha ili kukuza soko la ngozi nchini” amesema Hamisi.

Mafunzo haya ya wajasiriamali yanatajwa kuwa yenye tija zaidi kwani yatawaongezea ujuzi na maarifa kwa wajasiriamali hao lengo likiwa ni kuzalisha Zaidi na kukuza   uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *