Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Kenan Kihongosi ametoa siku 7 kwa wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani humo kumaliza ugonjwa wa Kipindupindu.
Aidha amewaagiza wakuu wa Wilaya na wakurugenzi Mkoani Simiyu kusimamia Sheria ndogo za Halmashauri kwa kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka kanuni za Afya na usafi wa mazingira ili kutokomeza kipindupindu Mkoani humo.
Mhe.Kihongosi ametoa rai hiyo katika kikao kilichokutanisha Viongozi kutoka Taasisi mbalimbali Mkoani Simiyu katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ulioko katika Mji wa Kiserikali Nyaumata Wilayani Bariadi kilichoketi kwa lengo la kujadili mikakati ya kupambana na ugonjwa wa kipindupindu.
“Hakuna aliye juu ya Sheria,tusioneane aibu,tuwajibike kutokomeza kipindupindu”Alisema Mkuu wa Mkoa Kihongosi.
Mhe.Kihongosi amesema kuwa baadhi ya Wanasiasa Mkoani humo wamekuwa wakikwamisha mapambano ya ugonjwa wa kipindupindu Mkoani Simiyu jambo linalochangia kuendelea kushamiri ugonjwa huo mkoani Simiyu.
Kutokana na changamoto hiyo,amesema hatofumbia macho kiongozi yeyote atakaekwamisha jitihada za Serikali katika mapambano ya ugonjwa hatari wa kipindupindu unaohatarisha maisha ya Wananchi Mkoani Simiyu.