RC DENDEGO ‘AZIFAGILIA’ NGO’s MIRADI YA UBORESHAJI HUDUMA KWA JAMII

Na Saulo Stephen – Singida.

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yamepongezwa kwa mchango wao mkubwa katika kuihudumia jamii, kupitia utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, huku yakihimizwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuleta maendeleo endelevu.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alipokuwa Mgeni Rasmi katika Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Singida lililofanyika katika Ukumbi wa RC Social, Manispaa ya Singida.

Dendego amesema mafanikio ya maendeleo yanahitaji nguvu na ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali na wadau mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa mashirika hayo kuhakikisha programu na miradi wanayoitekeleza inaendana na mahitaji halisi ya wananchi pamoja na mipango ya maendeleo ya Serikali.

Amesema mashirika hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha huduma za afya na lishe, kusaidia watu wanaoishi na VVU, kuchangia upatikanaji wa maji safi na salama, elimu, uwezeshaji wa kiuchumi pamoja na maeneo mengine ya kijamii.

“Mashirika yasiyo ya kiserikali ni mkono mkubwa wa kuisaidia Serikali katika kutimiza malengo yake. Mchango wa mashirika haya ni mkubwa; kazi inayofanyika wala haihitaji kuitafuta kwa darubini, ni kazi inayoonekana kwa macho ya nyama,” amesema Dendego.

Katika jukwaa hilo, lililokuwa na kauli mbiu isemayo, “Fikra Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani,” wadau walijadili namna ya kuimarisha uendelevu wa mashirika hayo kupitia ubunifu, ushirikiano na matumizi ya fursa za ndani katika upatikanaji wa rasilimali fedha.

Dendego pia ameyapongeza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mkoani Singida chini ya Mwenyekiti wao wa Mkoa, Happiness Francis, kwa kuendelea kuwa sehemu muhimu ya jitihada za kuboresha ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Taifa, Jaspar J. Makala, ameyataka mashirika hayo kuzingatia maadili ya uongozi katika kutekeleza majukumu yao na kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uadilifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *