Na Saulo Stephen – Singida.
Wananchi Mkoani Singida wametakiwa kuwekeza katika matumizi sahihi ya vyoo bora kwa kuhakikisha kuanzia ngazi ya vitongoji kila kaya inakuwa na choo bora, ili kujikinga na magonjwa yanayosababishwa na majitaka kama vile magonjwa ya tumbo pamoja na kipindupindu.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha kuhakikisha wananchi wa mkoa huo wanatumia vyoo bora katika makazi yanayowazunguka.
RC Dendego amesisitiza kuwa matumizi ya vyoo bora na usafi wa mazingira ni silaha muhimu dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mlipuko na hivyo kuwataka wananchi kubadili tabia hatarishi zinazochangia uchafuzi wa mazingira.

Aidha ameongeza kuwa matumizi ya vyoo bora ni vita halisi na makini hivyo kama mkoa watapambana kuhakikisha jamii yote ya mkoa wa Singida inakuwa vyao bora na hawatokubali kuona mtu yoyote anawarudisha nyuma katika kutimiza adhima ya matumizi sahihi ya vyoo bora.
Kwa Mujibu wa Takwimu inaonyesha kuwa asilimia 22 ya wakazi wa Mkoa wa Singida bado hawatumii vyoo bora au kutotumia vyoo kabisa, jambo ambalo Rc Dendego anasema halikubaliki, na kuwa kuwagiza viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji kusimamia matumizi sahihi ya vyoo bora.