
Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego ameshiriki katika zoezi la ukaguzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ambayo inategemewa kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru Mkoani humo ifikapo Julai mwaka huu 2025.
Dendego Amefanya ukaguzi huo akiambatana na Wajumbe wa kamati ya usalama wa mkoa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida, Sekretarieti ya Mkoa, Madiwani, Mwenyekiti wa kijiji, Serikali ya kijiji, Watendaji wa kijiji na wananchi.
Ziara hiyo iliyoanzia katika kijiji cha Pohama, imekagua ujenzi wa Ofisi ya Kijiji cha Pohama mradi wenye gharama ya Shilingi 66,400,000 ambapo shilingi 61,000,000 ni mapato ya ndani huku shilingi 5,400,000 ikiwa ni nguvu za wananchi Ujenzi uliokamilika.
Kadhalika umefanyika ukaguzi katika ujenzi wa nyumba ya Waalimu(2 in 1) katika Shule ya Msingi Pohama mradi unaotarajiwa kusaidia waalimu kuishi katika mazingira bora na kuwawezesha kuwa karibu na vituo vyao vya kazi,kuwapunguzia gharama za maisha na kuongeza motisha na usalama wa watumishi ambapo Mradi huu unatekelezwa kwa Shilingi 75,000,000 kwa mapato ya ndani huku 5,000,000/- ikiwa ni nguvu za wananchi.
Sambamba na hilo Mkuu wa Mkoa wa Singida amefanya ukaguzi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ngimu katika Tarafa ya Mgori,Kata ya Ngimu,Kijiji cha Ngimu linalojumuisha ujenzi wa Jengo la wazazi,Jengo la upasuaji,Jengo la Maabara,Jengo la kufulia,vyoo matundu 8,mfumo wa maji taka,kichomea taka,placenta pit,Ash pit,na uwekaji maji safi na umeme.
Awali akisoma taarifa,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Bi.Ester Chaula amesema Mradi huo unaotarajiwa kukamilika June 2025 unagharimu kiasi cha Shilingi 686,779,126 ambapo utasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya wenye uhitaji wa uangalizi na usaidizi maalumu kutoka katika kata za Ngimu,Itaja na maeneo jirani.
Pia umefanyika ukaguzi katika mradi wa ujenzi wa sanduku Kalavati la Mawe katika barabara inayounganisha Sagara-Pohama na Mgori ambapo ujenzi huo wenye gharama ya Shilingi 144,665,670 kutoka mfuko mkuu wa Serikali umewaepusha watumiaji kungojea masaa 2-4 kwa maji ya mvua kupita katika barabara sambamba na kuondokana na tatizo la kukwama na kushindwa kupita kwa watumiaji kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Aidha Dendego ametoa maelekezo kwa Uongozi wa Wilaya kuhakikisha wanakamilisha miradi yote kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu ili kuipa thamani fedha na matokeo yanayoonekana katika miradi hiyo huku akisisitiza utunzaji wa mazingira kwa kuhakikisha usafi unazingatiwa katika maeneo yote huku akiwataka wananchi kufika kwa wingi kuupokea mwenge wa Uhuru utakapowadia wilayani hapo kwa lengo la kuzindua miradi mbalimbali itakayoleta tija kubwa kwao.