RC CHACHA AJIONEA MAANDALIZI UTOAJI ELIMU YA VIPANDO VYA KILIMO NANENANE

Na Pascal Tuliano – Tabora.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amefanya ziara ya kukagua mabanda ya taasisi mbalimbali zinazoshiriki katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika katika viwanja vya Nanenane vilivyopo Ipuli Mnadani, Manispaa ya Tabora.

Katika ziara hiyo, Chacha amepata fursa ya kutembelea mabanda ya taasisi za biashara, mifugo, na vipando vya kilimo ambavyo vimeandaliwa kwa ajili ya kutoa elimu na kuonesha teknolojia mbalimbali zinazoweza kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo na ufugaji katika kanda ya Magharibi.

Maonesho ya mwaka huu kwa kanda ya Magharibi yamefunguliwa rasmi leo na mkuu huyo wa mkoa wa Tabora, yakihusisha washiriki kutoka mikoa ya Tabora na Kigoma huku yakilenga kuwapa wakulima mbinu mpya na bunifu za kuendeleza shughuli zao kwa tija zaidi. Maonesho hayo ni sehemu ya maadhimisho ya kila mwaka ya Nanenane ambayo huadhimishwa nchini kote kila tarehe 8 Agosti.

Wakati huo huo, maonesho ya wakulima kwa ngazi ya Kitaifa yamefunguliwa leo katika viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma ambapo yanashirikisha taasisi kubwa za kitaifa na kimataifa zenye mchango mkubwa katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Kaulimbiu ya Nanenane mwaka 2025 ni “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”. Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha wananchi kuchagua viongozi wanaojali maendeleo ya sekta hizo muhimu, kwa ajili ya ustawi wa taifa na kupunguza umasikini vijijini kupitia kilimo chenye tija.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *