Na Pascal Tuliano – Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amefichua wizi mkubwa wa Pamba unaofanyika kupitia uharibifu wa mizani janja iliyonunuliwa na serikali kwa ajili ya vituo vya ununuzi wa pamba mkoani humo.
Akizungumza akiwa Wilayani Igunga, Chacha amesema ukaguzi wa kina umebaini kuwepo kwa njama za viongozi wa vyama vya ushirika (Amcos) kushirikiana na mafundi vishoka kwa lengo la kuwaibia wakulima.

Kwa mujibu wa RC Chacha, Mkoa wa Tabora umepokea jumla ya mizani janja 186, ambapo mizani 105 imekaguliwa hadi sasa. Kati ya hiyo, mizani 36 imekutwa ikiwa imechezewa kimakusudi ili kupunguza uzito halisi wa pamba ya wakulima, hali iliyosababisha wizi wa kilo 1,043,294 za pamba zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500.
“Ni wazi kuwa huu ni mpango mahususi wa kuwaibia wakulima wetu,” amesema Chacha na kuongeza: “Mizani hiyo imekuwa ikifunguliwa kwa siri na baadhi ya viongozi wa Amcos wakisaidiana na mafundi wa mitaani, wakichezea mfumo wake wa kupima kilo ili kufaidika kwa njia ya udanganyifu.”

Kutokana na kubainika kwa wizi huo, Mkuu wa Mkoa ameagiza Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi 34 wa Amcos waliotajwa kuhusika, na kuhakikisha uchunguzi unakamilika haraka ili wahusika wafikishwe mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria huku Akisisitiza kuwa serikali haiwezi kuvumilia hujuma kama hiyo dhidi ya wakulima.
Aidha, Chacha ametoa onyo kali kwa mtu au kikundi chochote kinachojihusisha na uharibifu wa mizani au mali nyingine za serikali, akisema vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Tabora vipo macho na vitahakikisha kila mhusika anachukuliwa hatua kali bila muhali.


