Rais Ufaransa Avunja Bunge, Ujerumani Mambo Magumu

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ameamua kulivunja Bunge na kuitisha uchaguzi baada ya chama chake kushindwa vibaya katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya.

Akilihutubia taifa kutoka katika makazi ya rais ya Élysée jijini Paris, Macron amesema ameamua kurejesha chaguo la hatma ya bunge kupitia kura. Kwa hivyo analivunja Bunge la Taifa, uchaguzi utafanyika kwa awamu mbili Juni 30 na Julai 7.

Hatua hiyo ni baada ya duru kutoka Ufaransa kuonesha chama cha mrengo wa kulia cha National Rally kiko mbele zaidi katika uchaguzi wa bunge wa Umoja wa Ulaya, kuwashinda washirika wa Macron wanaounga mkono Ulaya.

Wakati Ufaransa mambo yakiwa hivyo, Matokeo ya awali ya bunge la Ulaya yanaonesha muungano wa Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz umeshindwa vibaya ambapo vyama vyote vitatu katika serikali yake vimekuwa nyuma ya vile vya kihafidhina na mrengo mkali wa kulia.

Matokeo hayo yanaibua wito kutoka kwa vyama vya upinzani vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union, CSU viliyomshinda Scholz wa mrengo wa kati kubadili mkondo au kuandaa uelekeo kwa uchaguzi mpya.

Upinzani unaongeza shinikizo ikiwa ni miezi michache kabla ya uchaguzi muhimu wa kikanda katika majimbo kadhaa ya mashariki ambapo chama cha mrengo wa kulia kinatabiriwa kuibuka na ushindi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *