Na Gideon Gregory – Dodoma.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 itakayofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete hapa Jjini Dodoma Januari 31,2025.
Akielezea tukio hilo leo Januari 29,2025 Msemaji mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa sera hiyo imelenga kuwa na wahitimu wenye maarifa, mwelekeo chanya na ujuzi unaoendana na mahitaji ya kitaifa na kimataifa utakao wezesha ushindani katika soko la ajira duniani.
“Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan mwezi Aprili,2021 alitangaza na kutoa maelekezo akitaka Wizara yenye dhamana ya Elimu ifanye kazi ya kupitia upya sera ya Elimu,
“lengo lilikuwa ni kuwa na sera itakayo waandaa wanafunzi wetu kuwa mahiri katika kukabiliana na changamoto za sasa na kujibu mahitaji ya dunia ya sasa, Mhe.Rais hakupendezwa kuona watoto wake wanakuwa na degree lakini hawana ujuzi katika uzalishaji na matokeo yake wanapatashida kwenye maisha yao,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa mapitio ya sera hiyo yanaakisi mahitaji ya kidunia na kutoa msukumo wa kuleta mageuzi katika sekta ya Elimu kwalengo la kuzalisha Raslimali watu wenyeujuzi katika ngazi mbalimbali kwa kujiajiri na kuajiri wengine.
Pia ametoa rai kwa watanzania kuhudhulia hafla hiyo pamoja na waliyoko katika mingine kushiriki kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Naye Katibu mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Carolyne Nombo ameeleza kuwa sera hutoa mwongozo wa uendeshaji na utolewaji wa Elimu Tanzania pamoja na mambo mbalimbali yanayowezesha utekelezaji wa sera hiyo ikiwemo mkakati wa sera husika huku akieleza kuwa mkakati huo umekwisha andaliwa.
Pamoja na hayo ameongeza kuwa sera itakayozinduliwa ilielekeza katika uboreshaji wa mitaala ya Elimu ambayo imeboreshwa kwa ngazi zote kunzia ngazi ya awali hadi hadi vyuo vikuu.
“Mitaala iliyoboreshwa inahusisha mitaala ya Elimu ya awali,mitaala ya Elimu ya msingi darasa la kwanza mpaka la sita,mitaala ya elimu ya sekondari ngazi ya chini na ngazi ya juu pamoja na mitaala ya mafunzo ya walimu.
Nifuraha kuwataarifu kwamba mitaala hiyo imekwisha anza kutumika mwaka jana na tayarui tumeanza kuona matokeo mazuri ya mitaala iliyoboreshwa,”amesema.
Amesema kutokana na dunia ya sasa kwendana na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia ambayo yanakua kwa kasi sana hivyo sekta ya Elimu imelazimika kwendana na mabadiliko hayo kwa kuandaa mkakati wa Tehama katika sekta ya Elimu pamoja na miongozo ya matumizi ya Tehama na akili unde.