Na Gideon Gregory, Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023 na Mitaala Iliyoboreshwa Januari 31,2025 Jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 10,2025 hapa Jijini Dodoma, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema Sera hiyo imeshaidhinishwa na Rais Samia kupitia kikao cha Baraza la Mawaziri.
“Sambamba na sera mitaala pia imefanyiwa mapitio na kubadilishwa ili kuendana na sera ambayo tunayo, kwasasa hivi tunayo mitaala mipya ambayo tunaitekeleza kwa awamu na suala hili ni kubwa na mageuzi yaliyopo kwenye sera ni makubwa sana,” – Prof. Mkenda.
Amesema mabadiliko hayo yataenda kugusa vizazi na vizazi kwani ukamilifu wa utekelezaji wake ni kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha Sita licha ya kuwa utachukua muda kwasababu walianza hatua kwa hatua na kuongeza kuwa yataenda kuleta muelekeo ambao utabadilisha taswira ya elimu nchini.
Prof. Mkenda amesema Serikali inasikia michango na hoja mbalimbali zinazotolewa na watu kuhusu Sera ya Elimu hivyo inaendelea kufuatilia ila majibu ya hoja zote zinazotolewa ziwepo ndani ya Sera hiyo.
“Mfano mjadala mkubwa unaoendelea kwasasa nchini ni kuhusu somo la Kingereza, ukienda kwenye sera utaona suala la lugha, ukienda kwenye mitaala utakuta ufundishaji wa lugha, tunasikia watu wanazungumza suala la akili mnemba ni suala kubwa sana lakini ukieda kwenye sera suala la tehama na mambo yote yanayohusiana na mambo haya yanayozungumzwa ukija kwenye mitaala utaona yanavyotekelezeka na kushughulikiwa,”amesema.
Pia mezungumzia suala la kufundisha ujuzi unaomuandaa mwanafunzi na dunia ya sasa na mabadiliko makubwa yanayotoka duniani kweda mbele sera hiyo inaelezea namna ya wanavyoshughulikiwa na mitaala inaeleza yanavyotekelezwa.