Rais Samia Suluhu Hassan leo 18 Septemba 2023 ameweka Jiwe la Msingi ujenzi wa Barabara ya Nachingwea–Ruangwa – Nanganga sehemu ya Ruangwa- Nanganga (km 53.2) inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Akizindua ujenzi wa barabara hiyo Rais Samia amesema serikali imejipanga kujenga miundombinu ya mikoa ya Kusini ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na kukuza uchumi wa mikoa hiyo na kuwataka wakandarasi wakamilishe ujenzi wa barabara hiyo kwa wakati.
Rais Samia amesema lengo la serikali ni kuunganisha mkoa wote wa Lindi kwa kiwango cha lami na wilaya kwa wilaya ziunganike kwa lami.
Akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa barabara hiyo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta amesema mkandarasi anayejenga barabara hiyo ni China 15th Group kwa thamani ya Sh bilioni 50.3 na jumla ya Sh bilioni 1.1 ikiwa ni sehemu ya ongezeko la thamani na kutumika kulipa fidia ya mali na ardhi kwa watu walioathirika na ujenzi kwa mujibu wa sheria.