RAIS SAMIA AWATAKA WATANZANIA KUJITOKEZA KUFANYA UWEKEZAJI NCHINI.

Na Saada Almasi -Simiyu

Watanzania wametakiwa kujitokeza katika kufanya uwekezaji mkubwa nchini kwani serikali imetengeneza mazingira mazuri ya wawekezaji kufanya kazi kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania.

Hayo yamebainishwa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wilayani Meatu mkoani Simiyu mara baada ya kuzindua kiwanda cha kuchakata pamba cha Biosustain Tanzania Limited kinachomilikiwa na mwekezani Riyadh Haidar ambacho tayari kimetoa takriban ajira 375 za kudumu na ajira zaidi ya 800 zisizo rasmi.

Rais Samia amesema kuwa viwanda vitamfanya mkulima aone faida ya kilimo anachofanya kwani kumwekea miundombinu rafiki ya kwenda kuuza malighafi zake kwa bei nzuri baada ya mavuno kunamtia moyowa kuzalisha zaidi.

“mapema hii leo nimezindua kiwanda kingine kikubwa hapa Meatu niupongeze sana uongozi wa kiwanda hicho kwa uwekezaji huo kwa sababu sasa mkulima anakwenda kufurahia mavuno yake kwa kuwa anapata faida kwanza hatosumbuka kufuata kiwanda lakini pia atauza malighafi kwa bei nzuri”amesema Rais Samia

“kama serikali ninawaahidi wawekezaji wote nchini kwamba tutaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili wengine zaidi wajitokeze,ninaamini ajira hizi 370 na zaidi zinazotolewa na kiwanda cha Biosustain zikitolewa na viwanda vingine tena na tena tutakuwa tumepunguza uhaba mkubwa wa ajira nchini”ameongeza Samia

Sambamba na hilo Samia amewapongeza wakulima wa zao la pamba wilayani humo kwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka kilo milioni 22 mwaka 2020 hadi kufikia kilo milioni 40 kwa mwaka 2025.

“nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuzalisha zao la pamba na mazao mengine lakini kipekee niwapongeze wakulima wa pamba wilayani Meatu kwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka kilo milioni 22na 700 mwaka 2020 hadi kufikia kilo milioni 40 hivi sasa”amesema Rais Samia

Rais Samia anaendelea na ziara yake ya siku tano mkoani Simiyu ambapo baada ya ukamilisha ziara yake wilayani Meatu ataenelekea wilayani Maswa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *