Katibu wa NEC itikadi,uenezi na mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi Paul Makonda amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ametenga siku moja kwa kila mwezi ili kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za mwananchi mmoja mmoja.

Hatua hii ya Rais inakuja ili kudhihirisha kwa vitendo tamanio lake la kuwataka watendaji wa serikali kutenga muda zaidi kusikiliza wananchi na kutatua kero zao mbalimbali.
Aidha Rais Samia pia ameamua kuja na utaratibu huo mpya kama sehemu ya kumuenzi hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyewahi kuwa na utaratibu kama huo wakati wa utumishi wake akiwa Rais wa Tanzania.
“Nitume salamu kwa watumishi kwamba umefika wakati mzuri ambao Mungu aliupanga. Wewe uliyepo ofisini na unamdharau mwananchi, atakapofika kwa Dkt. Samia akasema alienda kwenye ofisi ya fulani hakunipokea, alinifungia milango, alinitoa akanipa majibu haya na yale; kiama chako kinakugongea mlango’ – Makonda


