Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka mamlaka za upangaji miji Zanzibar kutenga maeneo maalumu ya michezo ya watoto ili kusaidia malezi bora na kujenga kizazi chenye maadili mema.
Rais Samia ameyasema hayo leo Agosti 12, 2026 wakati akizindua Kiwanja cha Kufurahishia Watoto katika Tamasha la Kizimkazi, akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa maeneo salama ya watoto kucheza na kujifunza.

Amesema baada ya maeneo hayo kutengwa, Serikali iwakaribishe wawekezaji kutoka sekta binafsi kujenga viwanja vya kisasa vitakavyowezesha watoto kupata mazingira bora ya ukuaji na maendeleo.
“Maeneo ya watoto yakitengwa yanakaa mwaka mmoja au miwili, baadaye unakuta matumizi mengine yameingia na eneo halipo. Kwa hiyo niagize kutengwa kwa maeneo ya kucheza watoto,” amesema.

Amesema viwanja vya michezo ni sehemu muhimu ya kujenga maadili, ubunifu na afya za watoto, huku akiwataka wazazi kutimiza wajibu wao wa malezi ili kuandaa kizazi bora kwa taifa.


