RAIS SAMIA ASEMA SERIKALI ITAIMARISHA MIFUMO YA MAAFA..

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa na kuhakikisha tunakuwa na utayari wa kukabiliana na dharura wakati wote.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo katika hafla ya chakula cha mchana pamoja na washiriki wa zoezi la utafutaji na uokozi wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa eneo la Kariakoo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati alipotembelea eneo la ajali mwezi Novemba, 2024.

Aidha, Rais Dkt. Samia ametumia hafla hiyo kuwashukuru wote waliojitolea katika zoezi la utafutaji na uokozi na amerejea msisitizo wake kuwa taarifa ya Kamati ya Uchunguzi wa ajali ya jengo kuporomoka Kariakoo itakapokamilika itawekwa wazi.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia ameridhia mwaliko wa Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo kufanya ziara katika eneo hilo la biashara kwa lengo la kuzungumza na wafanyabiashara wa eneo hilo.

Akijibu mwaliko kutembelea Kariakoo, Rais Dkt. Samia amesema atatumia ziara hiyo pia kuzindua ukarabati wa jengo la Soko Kuu la Kariakoo huku akirejea azma ya Serikali kulifanya soko la Kariakoo kufanya biashara kwa masaa 24.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *