Rais Samia aleta Mkeka mpya

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameanzisha nafasi ya Naibu Waziri Mkuu na kufanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri na makatibu wakuu wa wizara.

Aliyekuwa waziri wa Madini, Dotto Biteko ndiye Naibu Waziri Mkuu, akihusika na uratibu wa shughuli za serikali, pia anakuwa waziri mpya wa Nishati. Mara ya mwisho wadhifa wa Naibu waziri Mkuu ulikuwepo 1995 na kushikwa na Augustin Mrema wakati wa awamu ya pili ya uongozi ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Rais Samia pia ameifuta wizara ya Ujenzi na Uchukuzi badala yake ameunda wizara nyingine mbili, wizara ya Ujenzi na wizara ya Uchukuzi kama zilivyokuwa wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete. Aliyekuwa waziri wa Nishati January Makamba amehamishiwa Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Stergomena Tax amehamishiwa wizara ya Ulinzi alikohudumu awali.

Aliyekuwa waziri wa TAMISEMI, Angellah Kairuki amehamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii akibadilishana na Mohamed Mchengerwa. Balozi Pindi Chana aliyekuwa akihudumu katika Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo ndiye waziri mpya wa Katiba na Sheria, katika kipindi ambacho bado kuna vuguvugu la nchi kuwa na Katiba mpya na mabadiliko ya mfumo na sheria zinazohusiana na uchaguzi. Amebadilishana na Dkt. Damas Ndumbaro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *