Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza fedha za motisha kwa timu za Simba na Yanga kutoka Sh milioni 5 hadi Sh milioni 10. Atatoa fedha hizo endapo timu hizo zitafuzu kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Kombe la Shirikisho.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa leo Aprili 28, 2023 amesema magoli yatakayolipiwa shilingi milioni 10 ni yale yatakayofungwa katika dakika 90 za mchezo au dakika 120 na sio magoli ya penalti.
Amesema, Rais Samia anazitakia kila la heri Simba na Yanga na amewataka wachezaji kujituma uwanjani na kutumia maarifa yao yote kuhakikisha wanashinda michezo ya kukamilisha hatua ya robo fainali ili wafanikiwe kuingia nusu fainali, ambapo kila goli litakuwa shilingi milioni 10.
Simba inacheza mchezo wa marudiano leo Aprili 28, 2023 saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki dhidi ya Wydad Casablanca nchini Morocco, wakati Yanga watawakaribisha Rivers United ya Nigeria katika mchezo wa marudiano utakaofanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.