Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kazi ya kuondoa tope inaendelea na shughuli kubwa inayofanyika kwa sasa ni kufungua mitaa yote ya mji wa Katesh na kurejesha mji katika hali yake ya awali kwa kuwezesha shughuli za uzalishaji kuendelea.
Ameyasema hayo wakati akikagua kazi zilizofanyika ambapo aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista J. Mhagama, Waziri wa Madini, Antony Mavunde na Viongozi wengine , leo tarehe 6 Disemba 2023.
“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha leo kufikia usiku, mji wa Katesh na mitaa yake iwe imesafishwa ili kushughuli za uzalishaji ziendelee kama mnavyoona Wafanyabiasha wameanza kufungua Maduka” amesema Bashungwa
Bashungwa amesema TANROADS kwa kushirikiana na TARURA tayari ameweka mpango kazi wa pamoja ambao utahakikisha kazi hiyo inaendelea kufanyika usiku na mchana mpaka shughuli hiyo itakapokamilika.
Aidha, Waziri Bashungwa amevipongeza Vyombo vya ulinzi na Usalama, kwa kazi kubwa wanayofanya ambapo wamehakikisha wanaleta vijana wa JKT wanaoshiriki katika zoezi la uokozi ikiwa ni pamoja na kusaidia kazi za kurejesha hali nzuri katika mji wa Katesh.