Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia Wananchi kuwa Serikali inatenga kiasi cha Dola za kimarekani Millioni 10 sawa na Shillingi Billioni 300 kwa mwaka kwa ajili ya kulipa madeni ya Nchi.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa wakati Serikali inakopa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ina akaunti maalum inayoweka Fedha za kutosha Kulipa Madeni hayo ambayo sasa ina kiasi cha Shillingi Biliioni Mia Sita.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo wakati akifungua Kituo cha Mabasi Kijangwani kilichopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi kilichojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF).
Amefahamisha kuwa deni ililonalo Zanzibar kwa sasa ni Shillingi Trilion 1.2 linaloaminika na kuwa na uwezo wa kukopesheka tena kutokana na utaratibu huo uliopo Serikali inaweza kulilipa kipindi cha miaka miwili.
Aidha ameeleza kuwa Wakati Serikali ya Awamu ya Nane inaingia Madarakani deni la Serikali lilikuwa Shillingi Bilioni Mia nane na sasa baada ya miaka minne limepanda hadi kufikia Trilioni 1.2
Rais Dk.Mwinyi amekanusha vikali taarifa zilizotolewa na Wapinzani hivi karibuni kuwa Zanzibar ina deni linalofikia Trilioni 2.8 sawa na ongezeko la asilimia 208 kuwa za Uongo na Propaganda za Kisiasa zisizo sahihi.
Amesisitiza kuwa Serikali inakopa kwa nia njema ya Kuendesha Miradi ya Maendeleo yenye tija na maslahi kwa nchi na sio Vyenginevyo.
Akizungumzia kituo hicho kipya cha Mabasi ameutaka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ZSSF kuwa na Mpango maalum wa Matunzo na Usafi na kuandaa ajira Maalum kwa Vijana kwa ajili kutoa huduma hizo.