Raia wa Palestina Waukimbia Mji wa Rafah

Wapalestina waliojawa na hofu wameukimbia mji wa Rafah kabla ya majeshi ya Israel kuanza mashambulizi ya ardhini licha ya mazungumzo ya kusitisha vita kurejea tena huko mjini Cairo, Misri.

Licha ya jamii za kimataifa kupinga mashambulio hayo ya ardhini, Israel ilipeleka vifaru vyake katika mji wa Rafah na wanajeshi wake wakakikiteka kivuko kinachounganisha mji wa Rafah na Misri ambacho ni njia kuu ya kupitishia misaada kwenda katika eneo lililozingirwa la Palestina.

Ikulu ya Marekani imelaani kukatizwa kwa zoezi la utoaji wa misaada, huku afisa mmoja mkuu wa nchi hiyo akifichua kwamba Washington ilisitisha kuipelekea Israel shehena ya mabomu wiki iliyopita.

Hatua hiyo ilijiri baada ya mshirika wake huyo kushindwa kuihakikishia Marekani kwamba haitoendelea na mipango yake ya kufanya mashambulizi ya ardhini katika mji wa Rafah hata hivyo, saa chache baadae jeshi la Israel lilitangaza kwamba linakifungua tena kivuko cha Kerem Shalom, na kile cha Erez kwa ajili kuingizwa msaada mkubwa katika Ukanda wa Gaza.

Lakini licha ya kauli hiyo ya Israel, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina limesema kivuko cha Kerem Shalom ambacho Israel ilikifunga baada ya wanajeshi wake wanne kuuawa katika shambulio la roketi siku ya Jumapili bado hakijafunguliwa.

Vita hivyo vilianza tarehe 7 Oktoba mwaka jana wakati wanamgambo wa Hamas walipovuka na kuingia Israel kutoka Gaza, na Kwa Mujibu wa Takwimu za Israel katika mashambulizi yao watu wapatao 1,200 waliuawa na wengine zaidi ya 200 walichukuliwa mateka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *