Mshauri wa Rais Masuala ya Afya na Tiba ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Yakub Janabi ametangazwa rasmi kuiwakilisha Tanzania kwenye Uchaguzi wa kumpata Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika baada ya Mkurugenzi Mteule wa nafasi hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile kufariki.
Taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa WHO imeonesha kuwa Prof. Janabi ni miongoni mwa Wagombea watano ambao majina yao yatapigiwa kura kwenye mchakato wa Uchaguzi May 18, 2025.

Prof Janabi ni Mgombea pekee kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, huku wenzake wanne wakitokea nchi za Afrika Magharibi akiwemo Dkt. N’da Konan Michel Yao (Ivory Coast), Dkt. Dramé Mohammed Lamine (Guinea), Dkt. Boureima Hama Sambo (Niger) na Prof. Mijiyawa Moustafa wa Togo.
Mkurugenzi wa Kanda atachaguliwa kwa kura katika kikao cha ndani cha Kamati ya Kanda ya WHO kwa Afrika, ambayo ilikutana January 14, 2025, na kuamua kutumia utaratibu wa haraka, kumpata Mkurugenzi wa Kanda badala ya mchakato wa kawaida ambayo huchukua muda mrefu.


