Na Gideon Gregory – Dodoma.
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), imeeleza kuwa inaendelea kuimarisha usimamizi wa ununuzi wa umma nchini kwa kutumia mifumo ya kidijitali, ikiwa ni sehemu ya kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya fedha za Serikali.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mfumo wa ununuzi wa umma leo Agosti 20, 2026 Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Denis Simba amesema, mamlaka hiyo ina jukumu la kusimamia na kudhibiti utekelezaji wa sheria za ununuzi wa umma, na si mamlaka inayotoa zabuni zote za Serikali.

“PPRA inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria mpya ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023, ambayo inalenga kuimarisha usimamizi wa michakato ya ununuzi wa umma pamoja na kuongeza uwajibikaji kwa watendaji wanaohusika na matumizi ya fedha za umma,” amesema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, takribani asilimia 70 ya bajeti yote ya Serikali inatumika kupitia ununuzi wa mali, huduma na kazi za umma, hali ambayo inaonesha umuhimu wa kuwepo kwa mfumo imara wa ununuzi unaohakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria.
“Aidha, PPRA inasisitiza umuhimu wa kuwa na viongozi na watendaji bora wenye uelewa mahsusi wa mfumo wa ununuzi wa umma, ili kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa na fursa za ununuzi zinawafikia wadau mbalimbali kwa usawa,” amesema.
Ameongeza kuwa, PPRA inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na matumizi ya nyaraka za kughushi katika michakato ya ununuzi ambapo kupitia maboresho ya mifumo na usimamizi madhubuti, inatarajia ndani ya mwaka huu kupunguza kwa kiasi kikubwa na kuondoa, matumizi ya nyaraka za benki za kughushi katika michakato ya zabuni.
Kwa upande wa wanufaika wa mfumo wa ununuzi wa umma, Elizabeth Kasimira, ambaye ni Mwenyekiti wa Kazi Iendelee Group, ameeleza kuwa matumizi ya mfumo huo yanawapa fursa wadau kushiriki katika zabuni za Serikali kwa njia rahisi na yenye uwazi zaidi.
“Kundi letu limefanikiwa kupata zabuni 21 zenye thamani ya shilingi bilioni 2.1 niwaombe wanawake, vijana na wazee kutumia fursa zinazopatikana kupitia mfumo wa ununuzi wa umma na kushiriki katika zabuni zinazotangazwa badala ya kuachwa nyuma katika fursa za kiuchumi zinazotokana na matumizi ya fedha za umma,” amesema.


