Na Gideon Gregory- Dodoma.
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), imezuia utoaji tuzo wa zabuni 43 zenye thamani ya kiasi cha shilingi Bilioni 586 kwa Wazabuni waliokosa uwezo wa kifedha na sifa za kitaalamu zinazohitajika kutekeleza zabuni husika.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Februari 25,2026 Jijini Dodoma Mtendaji wa PPAA, James Sando amesema hatua hiyo imezuia utekelezaji usioridhisha wa miradi, ambao ungesababisha upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo endelevu na stahiki kwa wananchi.

“Kwa hivyo, hatua ya Mamlaka ya Rufani kuzuia utoaji wa tuzo kwa wazabuni 43 waliokosa sifa za kutekeleza zabuni, inaimarisha mchakato wa usuluhishi wa migogoro moja ya falsafa nne za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.
Aidha, amesema Serikali inaamini kuwa usuluhishi wa migogoro hauwezi kufanikishwa katika mazingira ya ubaguzi wala pale ambapo fursa na haki za kiuchumi na kiraia hazitolewi kwa usawa.

Mbali na hayo Sando amesema katika kuendeleza azma ya Serikali ya kuimarisha uwazi, uwajibikaji, na ufanisi katika sekta ya ununuzi wa umma hususani ushughulikiwaji wa malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma, Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na PPRA imekamilisha ujenzi wa Moduli ya Kupokea na kushughulikia Malalamiko na Rufaa zinazotokana na michakato ya Ununuzi wa Umma.
“Moduli hii ipo katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST), na inatoa njia rahisi, ya haraka, na yenye uwazi kwa wadau wote kushiriki katika mchakato wa usulushi wa migogoro ya ununuzi. Hii inachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha utendaji na kuimarisha imani katika mfumo wa ununuzi wa umma,” amesema.

Pia ameongeza kuwa hadi sasa, jumla ya malalamiko 549 yamewasilishwa na kushughulikiwa na taasisi nunuzi kupitia Moduli hiyo, jambo linaloonesha mwitikio chanya kutoka kwa wazabuni na taasisi nunuzi katika kutumia mfumo huo kwa ajili ya kupokea, kuchambua na kutoa maamuzi kuhusu malalamiko yanayohusu michakato ya ununuzi wa Umma.
“Aidha, jumla ya rufaa 26 zimewasilishwa na kushughulikiwa na Mamlaka ya Rufani kupitia moduli hiyo, hatua ambayo imeongeza ufanisi katika usimamizi wa rufaa, kupunguza muda wa kushughulikia mashauri, na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa haki,” ameongeza.