Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Wafanyabiashara wa jiji la Dar es salaam wamekaribishwa kuwekeza katika Pori la akiba pande katika sekta ya utalii kwa kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori (TAWA) imetenga maeneo mahsusi kwa ajili ya uwekezaji katika miundombinu ya michezo ya watoto yenye kiwango cha kimataifa pamoja na ujenzi wa huduma za malazi.
Wito huu umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula alipokuwa akijibu swali la Mhe. Mariam Nassoro Kisangi Bungeni jijini Dodoma kuwa Serikali ina mpango gani wa kuliendeleza Pori la Pande lililopo jijini Dar es salaam kuwa Kivutio cha Utalii.
Aidha Mhe. Kitandula amesema kuwa Kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022, Wizara ilijenga miundombinu mikubwa ya maeneo ya kupumzikia wageni (Picnic Sites) na kambi za watalii (Public Camp Sites) katika eneo hilo.
Vilevile ameongeza kuwa kwa mwaka 2023/2024 Wizara hiyo imeanzisha bustani ya wanyamapori na kuweka wanyama katika eneo hilo ambapo mpaka sasa, pori hilo lina idadi ya wanyamapori zaidi ya 100. Aina za Wanyamapori waliopo sasa ni duma, mamba, simba, pundamilia, nyumbu, swala granti, swala pala na nyoka wa aina mbalimbali akiwemo chatu.
Mhe. Kitandula amesema kuwa miundombinu ya barabara katika Pori hilo imeboreshwa na inapitika katika kipindi chote cha mwaka na Wizara imejenga lango kuu la kuingilia kwenye pori hilo kwa Kufuatia juhudi hizo, idadi ya watalii wanaotembelea pori hilo imeongezeka ambapo kuanzia mwaka 2023 hadi 2024 watalii walifikia 4,606.